Mfanyi kazi ana mengi ambao huvunja moyo hata baada ya kutia bidii katika kazi yake kwa mwajiri. Huteswa na kupitia mengi ya dhuluma, lakini kwa mwajiri wake bora tu amsaidie kupat riziki yake. Tazama shairi hili… Mwajiri una Dhuluma


Mwajiri una Dhuluma

Nimetenda ya huduma, japo machungu nameza,
Ya suluhu nasukuma, malipo hujaongeza,
Nakupachika lawama, sinalo la kunyamaza,
Mwajiri una dhuluma, unatenda ya kubeza.

Unawania kuvuma, kishujaa watokeza,
Kwa anasa umezama, kwingine yanapooza,
Kutoa inakuuma, bilioni wawekeza,
Mwajiri una hujuma, unatenda kuchukiza.

Mwanangu ashika tama, maakuli akiwaza,
Hana lake vazi jema, ya maisha yamkwaza,
Kwa kilio hajakoma, asijue kueleza,
Mwajiri huna hishima, unatenda yenye kiza.

Mwalimu hana la wema, kwa karo sijamtuza,
Mwanangu amemtuma, hasomi anampuza,
Ni muhali la kusoma, mwanangu akaongoza,
Mwajiri si taadhima, unatenda ya kutweza.

Mwanangu anaye mama, mke hajanitukuza,
Kila siku akoroma, fitina ameikuza,
Kazi hiyo nikahama, heri nende kuchuuza,
Mwajiri unavyouma, unatenda kuumiza.

Mwenye nyumba alalama, kumlipa sijaweza,
Mengi yake amesema, kwa kishindo anikaza,
Anadai darahima, kwa sasa hajaliwaza,
Mwajiri huna huruma, unatenda kuchokoza.

Nina madeni ya vyama, riba imejiongeza,
Hakuna langu la wima, yote nayotekeleza,
Imefifia neema, mambo navyopeleleza,
Mwajiri huna rehema, unatenda kutatiza.

Mimi sina kwangu kwema, kila kitu nimeuza,
Yangu yote yamekwama, umefifia mwangaza,
Ninasubiri Karima, aondoe kiambaza,
Mwajiri una hatima, unatenda kufukuza.

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

*