Ulinizalia Nini?

Swali ninakusaili, wewe uliyenizaa
Mbona usinikubali, mwanao nimeduwaa
Ulofanya ukatili, hata nzi wamezubaa
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Starehe za mahaba, kasahau u mdogo
Wavuli hadi wababa, kawapa penzi kidogo
Wengine wakakukaba, ukawa kama kigogo
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Sasa ninatapatapa, kana kwamba ni yatima
Sili kipande cha papa, kwa sababu yako mama
Mlo naula kwa pupa, nisije pata dhuluma
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Shati labgu ndilo mto, vibarazani nalala
Natafuta hata moto, baridi isije nila
Kelele za watoto, polisi na zao ala
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Nishapatwa na maradhi, kohozi hadi upele
Mara ni barabarani, sina nyuma wala mbele
Naitwa hayawani, kwani shida zangu tele
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Rabuka akusamehe, mamangu umenitosa
Nalia sina sherehe, silijui langu kosa
Wakati sija balehe, tena watu waniposa
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

Tamati nimefikia, nisije nikakufuru
Kilio umesikia, hata uwe Buruburu
Nakushukuru Jalia, nimewashibda kunguru
Ulinizalia nini, kama hungenileaa

© Emmanuel Charo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *