Kuni Motoni

Kuni juu ya uchaga, hucheka zilo Motoni,
Mzinga una masega, na uki bado u ndani,
Tazifunga zangu njuga, sakate bila utani,
Mtafitafi ale swi, mtulivu hula nyama.

Mtego usio chambo, haunasi kitatange,
Ukinitaka kimombo, nitasema na niringe,
Nichezeshe langu tumbo,samaki nimkaange,
Ajimegea makubwa, kumbuka siku kulima.

Mpiga maji makanda, huvuja kwa makwapani,
Kichapo kuzidi punda, kuteseka akilini,
Nimeshindwa kuupanda, kuanzia kileleni,
Kutwanga na nisikule, nazuia mchi wangu.

Kitaka kula uhondo, nawe utie matendo,
Nyatanyata kandokando, usipate na ‘mpondo’,
Ushike vyema upondo, ulenge bila ya kando,
Kazi huvunjwa na kazi, mtu huzila nguvuze.

Fundi mubaya huteta, huteta na ala zake,
Sitayazua matata, uwelewano tusake,
Kifikia yangu nyota, sitalipa kwa mateke,
Ala! Mchele ni mui, swali ni wapishi nao?

Mzingeni si fungeni, na lao hawalioni,
Silaumu mashakani, ulishika kiunoni,
Ukadharau jichoni, kunibedua domoni,
Anayeweka kikaka, hupanda shamba na taka.

Na mavi usiyoyala, wayawingiani kuku?
Nyingi zangu umekula, hivyo ndivyo nakushuku,
Ni wakati wa kulala, mi ndege mie Kasuku,
Anayemulika nyoka,huanzia miguuni.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *