Kauchonge Mzinga

Ewe mrina asali, upendaye kupakua,
Bila hata kusaili, wala kutaka tambua,
Ninakuonya badili, mapema hiyo tabia,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

Kajichongee mzinga, wa kwako ewe fulani,
Au takatwa mapanga, ya kifua na kichwani,
Ujute kama kipanga, aliyenaswa bandani,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

Usiku wanyemelea, asali kwenda pakua,
Wadhani hatujajua, ujanja unotumia,
Sikuyo yaja sikia, bila maji takunyoa,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

Asali we kuipata, ni lazima kujipanga,
Kwanza ni mti kukata, kwa shoka au kwa panga,
Halafu mundu kamata, mzinga uanze chonga,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

Ukishachonga vizuri, uutundike mtini,
Penye maua mazuri, waridi na asumini,
Halafu wewe subiri, nyuki taja mzingani,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

Mimi hapo naachia, ukweli nishakwambia,
Usije kupuuzia, mwishowe ukajutia,
Ulie ungalijua, mijino kujisagia,
Kachonge wako mzinga, upakue utakavyo.

© Bonface Wafula
(Mwana Wa Tina) Lanet, Nakuru.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *