Lahaja za Kiswahili

Leo ninazama ndani, nikazitaje lahaja,
Za lugha hino ya shani, ya fahari na natija,
Nazipanga kwa foleni, kizitaja moja moja,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Ninaanzia Unguja, kisiwani Tanzania,
Twakipata Kiunguja, ambacho kimeenea,
Hino ndo kubwa lahaja, wengi wanoitumia,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Pia kunacho Kiamu, chatumika Lamu sana,
Sisahau Kihadimu, Tanzania kule bwana,
Lahaja zenye utamu, ninawajuza wangwana,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Kunacho Kimtang’ata, Kule Tanga Tanzania,
Pia kweli takikuta, Kimafia cha Mafia,
Pamoja na Kimvita, Mombasani nawambia,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Nenda kisiwani Pemba, huko takuta Kipemba,
Kote kote kinatamba, kama wa porini simba,
Na pia kuna Kivumba, kwenye kisiwa cha Vumba,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Kingwana sijasahau, kule Kongo nduzanguni,
Pia kunacho Kisiu, pia nacho Kibajuni,
Pamoja na Kitikuu, kisemwacho Mombasani,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

Kingazija na Kingozi, Kipate na Kimrima,
Sisahau Chibalonzi, kule pwani wakisema,
Kutaja zote siwezi, zimetosha nasimama,
Lahaja za kiswahili, nataja tuzitambue.

© Bonface Wafula (Mwana wa Tina)
St. Monica Lanet, Nakuru

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *