Udugu Hazina Yetu

Udugu ndio hazina, alopewa kila mja,
udugu wa kupendana, ukizio zetu haja,
udugu uso hiana, ndio undugu wa tija,
Udugu hazina yetu.

Udugu ni kushikana, pamoja kwa kila hali,
udugu kujuliana, wote tujuane hali,
udugu si kutengana, hata kama tupo mbali
Udugu hazina yetu.

Udugu sio kuringa, kisa mejaliwa kitu,
udugu si kujitenga, ndugu umuone chatu,
udugu huu naronga, udugu sifa ya utu,
Udugu hazina yetu.

Udugu ni kushiriki, sote tuyale matunda,
udugu si uzandiki, nyoyo kuzijaza inda,
udugu wa kinafiki, hata Mola auponda,
Udugu hazina yetu.

Udugu ni kufaana, ndo agizole Manani,
Udugu ni kupendana, kioo kwa majirani,
udugu wa kugombona, huo ni wa kishetani,
Udugu hazina yetu.

Udugu wenye nidhamu, ndio udugu wa kweli,
Udugu wa kumweshimu, hata asiye na mali,
Udugu huu mtamu, shubiri huwa asali,
Udugu hazina yetu.

Udugu tuutunzeni, hii ndo hazina yetu,
Udugu tuushikeni, hata kati ya msitu,
Udugu ‘japo wageni, basi wajifunze kwetu,
Udugu hazina yetu.

© Marko John Kinyafu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *