Buriani Babu

Yadidimia miezi, miaka itafunguka
Usiseme ni upuzi, ila mi nahangaika,
Zatingika zangu fizi, kwa moyo mengi mashaka,
Buriani wangu babu.

Hekimayo ya kuiga, ‘hina’ wa kumithilishwa,
Kanipatia masega, na uki wa kurambishwa,
Kwa vitendo kanifuga, yaso mawi kuonyeshwa,
Buriani wangu babu.

Maisha kawa ucheshi, kiwa kwetu mashambani,
Ngano zako za ujeshi, na Vita vya ukoloni,
Livyosimama marshi, kutoa Kenya ‘komboni’,
Buriani wangu babu.

Nakumbuka kikariri, livyojawa na majuto,
Maisha liwa shubiri, ujana wako wa moto,
Hukuficha yako Siri, livyong’olewa makato,
Buriani wangu babu.

Ningekuwa na uwezo, ngekwamsha lipolala,
Ulikuwa yangu nguzo, kunifunza njema Sala,
Nayatilia mikazo, mazuri yako makala
Buriani wangu babu.

Sioni soni kinena, kuwa u wangu shujaa,
Msijaribu kukana, msizwe kwangu balaa,
Wakuwahi babu sina, babungu wangu mkaa,
Buriani wangu babu

Taacha kukulilia, nianze kufurahia,
Kiticho nitakalia, shairi kukutungia,
Nasaha tafwatilia, mengi nitahifadhia,
Buriani wangu babu.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *