Nani Kama Mama

Titi la mama litamu, jingine halachi hamu,
Hupa akili timamu, la lea hamu na ghamu,
Lafunza yalo muhimu, vile maji sio damu,
Aha! Nani kama mama, hakuna kama mama.

Nyingi tungo watungiwa, barani na baharini,
Kuna mengi huambiwa, kwa mandishi na vinywaji,
Nayo hamu kuishiwa, nakataa abadani,
Aha!Nani kama mama, hakuna kama Mama.,

Kwenye chupa akabeba, kitoto kijusi mie,
Kanizaa kwa mahaba, asitake nangamie,
Akateseka si haba, toto mie lisilie,
Aha!Nani kama Mama, hakuna kama mama.

Pajani kunipakata, mikono kunieleka,
Nikayazua matata, ‘kupewa’ nilichotaka,
Nikizua vingi Vita, penzi lake likashika,
Aha!Nani kama mama, hakuna kama mama.

Akabanika kiazi, sharti kunikatia,
Ya pwani kikuna nazi, lipenda kunipatia,
Akifanya yake kazi, linibeba katulia,
Aha!Nani kama mama, hakuna kama mama.

Beti zangu hizi sita, za mama kumsifia,
Atakaye zangu Vita, kwa mama kudhulumia,
Laana atazipata, hakika atajutia,
Aha!Nani kama Mama, hakuna kama mama.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati).

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *