Tenda Wema Uondoke

Ndugu jiulize swali, swali lataka hekima,
Hekima kwa yako hali, moyo na ungesimama,
Wangekukumbuka kweli, nijibie himahima,
Tenda wema uondoke, usitake washukuru.

Shujaa yule wa kale, alokuwa wetu Simba,
Tulipiga tu vigele, sifaze zilizotamba,
Tukampa sifa tele, alipoikata kamba,
Tenda wema uondoke,usitake washukuru.

Nawe ulisaidiwa, je ulisaidia?
Mazuri ulipangiwa, swali,uliwapangia,?
Busara ulipatiwa, aha!Uliwapatia?
Tenda wema uondoke, usitake washukuru

Mwanadamu hawezani, kumlipa mwanadamu,
Wa kulipa ni Dayani, hulipa bila shutumu,
Hebu tia maanani, Mungu tu ndiye karimu,
Tenda wema uondoke, usitake washukuru.

Kungekuwa na waziri, mawaziri wa uhai,
Wangekuwa machakari, kututenda ya jinai,
Tusingepata hadhari, maisha ni jitimai,
Tenda wema uondoke, usitake washukuru.

Mwenza nimefika mwisho, jawabu sijalipata,
Limenichosha najasho, mejiongeza matata,
Nipe jibu lako kesho, fikiria utapata,
Tenda wema uondoke, usitake washukuru.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *