Kipepeo

Nilikusaka chakani, bondeni na milimani,
Nikapandia mitini, nikadungiwa mibani,
Nikalia upeponi, na machozi ya juani,
Kipepeo kapepea, ukaenda mauani.

Niliimba tamu nyimbo, za mapenzi nyimbo tamu,
Nyingi zilijawa fumbo, kitaka zikupe hamu,
Wameta wako urembo, nilitaka ufahamu,
Ila mwanzo hukupenda,kusikia nilosema.

Nikakwahidi hidaya, kitaka we unipende,
Neleze bila ubaya, nilitaka nikuwinde,
Hazitabaki hekaya, hemko lisikupande,
Hila kwako zilibidi, ndo ujue likupenda.

Upolewo liniteka, huruma ukanipamba,
Kuondolewa mashaka, ya moyo yalonitamba,
Na mema yalifunguka,yakafanya niwe Simba,
Nilitona langu chozi, pindi uliponasika.

Kipepeo nakupenda, penzi nalo la ukweli,
Mazuri nitakutenda, u karibu uwe mbali,
Nitaishi kukulinda, moyo na kwa wako mwili,
Penzi ili ling’arike, lataka useme wazi.

Wanadamu wana hamu, yakuleta nyingi chuki,
Weleze wana wazimu, wacheze na sisi nyuki,
Tutawadunga kwa simu, kamwe wasirambe uki,
Wenye wivu wasikie, na wameze wote wembe.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *