Nawaita Magunge

Nawataka na magunge, wajenifunza kutunga,
Napo tunga nizitunge, zilotungwa kama shanga,
Mishororo niipange, pasi wazo kubananga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.

Kuandika Natamani, tungo zisizo ngenga,
Ziridhi ja asumini, kila mara nikipanga,
Nijesifiwa jamani, kuwa naitunza kunga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.

Niyachezee maneno, kama bisi na karanga,
Mizani iunde neno, lau uzi kwa kitunga,
Nitunge hata na ngano, pasipo wazo kuvanga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.

Nitunge zilo jadidi, si kama za vijulanga,
Mahuluku niburudi, pasina kuhangahanga,
Daima nijitahidi, niwache kuungaunga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.

Beti tano za kamili, namalizia kutunga,
Galacha niwakabili, wanirudi kijulanga,
Wanijazie akili, wizani usinichenga,
Na waje walo magunge, njia kunimulikia.

Moses Chesire
Sumu Ya waridi
Kitale

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *