Ulimi Kiungo Dhaifu

Ulimi kiungo dhaifu, kitumie kwa makini,
Kipe tosha marukufu, kisikuweke motoni,
Kisikupe udhaifu, ueleke kaburini,
Kingo kidogo Ulimi, maneno yake upanga.

Kingo kidogo ulimi, maneno yake upanga,
Tutumie zetu ndimi, vyema maneno kupanga,
Kunena maneno kumi,wacha yawe yenye mwanga,
Gizani tuonekane,kwa nuru ya ndimi zetu.

Gizani tuonekane, kwa nuru ya ndimi zetu,
Hata usiku manane, dhihirike wetu utu,
Maneno yetu tokane, na nzuri fikira zetu,
Tusiwe ja hayawane, kunena bila busara

Tusiwe ja hayawane, kunena bila busara,
Kalamu yangu mashine, hijamala kuparara,
Wosia wangu napene,kwenu siwe masihara,
Ulimi jamani Ulimi, utumike kwa hekima.

© Vincent Okwetso

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *