Siku Yangu Ikifika

Siku yangu ikifika, nirejee kwa Dayani,
Wanangu watasumbuka, niwaache kilioni,
Wengi watahuzunika, machozi yawe machoni,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Ole,watakoshituka, nikikwisha safiria,
Watabaki wakimaka, mesonga pasi kwambia,
‘Sijue pa kunisaka, deni lao kulipia,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Kuna wengi watafika, kuona jeneza langu,
Na wengine wakitaka, kutazama sanda yangu,
Inisi hawatachoka, kulongana hali yangu,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Naomba kufahamika, na hawa nawatambua,
Na watakaojazika, wali, pure kuchimbua,
Hata sima watataka, pamoja na vitumbua,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Kunao watapangika, kukagua yangu nyumba,
Milango itafunguka, ‘wachungule’ kwenye chumba,
Hawatawa na haraka, kulizuru hata shamba,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Ninalo la kuwataka, mjichunge nao hawa,
Wale watakaotaka, wana wangu kuachiwa,
Watoto kutaabika, nitarudi kuwaua,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Mie mekwisha andika, siku yangu ikifika,
Kimaliza kunizika, nitawa nimeondoka,
Niende kupumzika, pamoja na malaika,
Dhiki zitabaki kwenu, mie sitayafahamu.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *