Maisha Kalamu

Kalamu huundwa nzima, hitamani ipunguke,
Na yapenda kujituma, kufanya ihangaike.

Maisha ni kuyaishi, ni mambo yanayoisha,
Kwona mengi ni kuishi, tajiriba kuwapasha.

Maisha ni kuyachonga, ja kalamu ya kwandika,
Kujitolea mhanga, kuishi kwa kudhulika.

Kuishi kuna machungu, hali hii na nyingine,
Ili kuchora kifungu, kalamu ‘ chongwe’ machine.

Uishi kutenda mema,wenzako kuwafaidi,
Watakutilia hima, wakutende ukaidi.

Kulala njaa kwa leyo, itawa shibe ya kesho,
Kuwa ja kalamu hiyo, jiundie mwema mwisho.

Mwenza kuishi yabidi, kung’ang’ana ja kalamu,
Na ni leo toka Jadi, kuumizwa yalazimu.

Nikifunga zangu beti, mja Mungu kurehemu,
Usiishi kwa laiti, Maisha kama kalamu.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *