Heri Nirudi Shambani

Napiga yangu akili, ninatafakari sana,
Kulihusu jambo hili, linonisumbua sana,
Meshindwa kulihimili, lanilemea naona,
Heri nirudi shambani, waliko wazazi wangu.

Heri nirudi Musamba, kule nilikozaliwa,
Nikalime letu shamba, nikajipandie miwa,
Nepuke yanonikumba, hapa mjini wapendwa,
Heri nirudi shambani, waliko wazazi wangu.

Nende kwa mamangu Tina, anipikie ugali,
Wa muhogo kwa omena, na uji wa kiasili,
Vya mjini kwepukana, vyakula vya kemikali,
Heri nirudi shambani, waliko wazazi wangu.

Humu mjini taabu, humu mjini mashaka,
Maji safi ni taabu, chakula ni shida kaka,
Kodi nayo masaibu, kila siku yongezeka,
Heri nirudi shambani, waliko wazazi wangu.

© Bonface Wafula
(Mwana wa Tina) Lanet, Nakuru

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *