Nawauliza Waganga

Jana ndoto linijia, kote kumejaa damu,
Sijui likotokea, tena yao binadamu,
Mana nalisubiria, meuliza wanajimu,
Waganga naulizia, kitale lama lamu.

Ngeu ilitapakaa, aridhini na maweni,
Mito nayo ikajaa, ikamwaga baharini,
Sijaona tena baa, ‘lohiliki taifani,
Waganga naulizia, kitale lama lamu.

Insi walijifia, mabondeni na nyikani,
Jasadi zikabakia, kuliwa na hayawani,
Sijui yao hatia, lopeleka kuzimuni,
Waganga naulizia, kitale lama lamu.

Tama nikajishikia, mafuvu ‘lipoyaona,
Nika’nza kuriaria, moyo upate kupona,
Tena nikapiga dua, nikimusihi rabana,
Waganga naulizia, kitale lama lamu.

Nakaona wanijia, visu vikimeremeta,
Toba nikajililia, nikinywea nikitweta,
Macho akitumbua, nikajua kimepata,
Waganga naulizia, kitale lama lamu

Mara nikashitukia, kokoiko ya kikwara,
Ndotoni sikufia, wala mkuki kugwara,
Lakini najiwazia, walikuwa makafara?
Waganga naulizia, kitale lama lamu

© Moses Chesire
(Sumu la waridi) Kitale mjini

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *