Nakurejelea Rabuka

Nashukuru usokoma, hapa nilipopafika,
Moyoni nina naima, tena isomithilika,
Ulonitenda ni mema, ewe uliye rabuka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Baba tokea azali, jinalo limesikika,
Ila miye sikujali, kikweli sikulitaka,
Sasa nimeyaratili, ndiposa ninakusaka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Nimevuta afyuni, moshi pia kinifuka,
Nikafanya ya kihuni, ovyo nikisepetuka,
Leo nimeketi chini, izara zikinishika,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Vituko madanguroni, jahara yalifanyika,
Nilofanya vitandani, soni inanighubika,
Ila tijara sioni, uzee ninapofika,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Nikafanya uchopezi, nikiwa sugu kibaka,
Kuamini huyawezi, hili ni jambo hakika,
Sasa natoa machozi, hayo nikiyakumbuka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Kila kitu kitakoma, siku hiyo ikifika,
Siku hiyo tasimama, mbele ya baba Rabuka,
Nataka kuweza sema, dhambi nimeziepuka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Anasa nilishiriki, zimegeuka dhihaka,
Imenizulia dhiki, tena sizomithilika,
Ina chachu kama siki, tena chafu kama taka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

Beti nane namaliza, nimesema kwa hakika,
Dhambi tena sitasaza, kaburini nazizika,
Amri sitozicheza, wala tusi kutamka,
Nakurejea Rabuka, mimi wako mpotevu.

© Moses Chesire
(Sumu ya waridi) Kitale mjini

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *