Hajui Kupenda

Mahaba kitu kitamu, tamu kwa mwenye kupenda,
Hasa kwa ule msimu, wa penzi lenu kulinda,
Kila wakati ni simu, za habari za kushinda,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui,

Mapenzi ni tendawili, hujui kuitegua,
Ukiwaza marambili, hujui la kutatua,
Hasa kwa kiwiliwili, cha kwako kikitulia,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

Utashindwa na kulala, ukilala wa mang’amu,
Uchore mengi makala, ukiwaza penzi sumu,
Usahau hata kula, kwenye nyumba na kalamu,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

Picha yako penzi chako, witazama tabasamu,
Sebule na kwenye jiko, i juu kwenye fremu,
Kinywa chajaa kicheko, penzi kutia wazimu,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

Popote kwa mahasibu, ni hadithi za mapenzi,
Ng’o huwezi kuwa bubu, wagana za penzi tenzi,
Wamtamani mhibu, na kwa pamoja ‘mdanzi’
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

Wakuja kitabasami, moyo raha bila dhiki,
Unakuja wajihami, kwa chokoleti na Keki,
Umpendaye hasemi, penzi lako haafiki,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

Wamwandikia barua, zenye tungo za mapenzi,
Akipata ararua, kukufanya we mshenzi,
Hiyo ndio shukuria, mpenzi asokuenzi,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui

Tiba ya penzi kupenda, kwa kutenda kutendana,
Asopenda hatatenda, ju ya chuki kupandana,
Liko huzuni kutanda, basi heri kutengana,
Ila ni anayependwa, kupenda naye hajui.

© Mwangi wa Githinji
( Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *