Sioni Raha Mkata

Mkata sina rafiki, kila mja ni adui,
Nguo moja namiliki, nivaayo sikatai,
Ingawa mwanihakiki, kama mie hunywa chai,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

Niendapo kibarua, asubuhi na mapema,
Nyie mwanifuatilia, mjue ninakolima,
Baada ya kupajua, mnaanza kunisema,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

Mkimuona mwanangu, mararu kayavalia,
Hamwezi hisi uchungu, kinaya mwafurahia,
Kweli nyie walimwengu, Rabuka kawangalia,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

Muonapo nina kuku, mnadhani nimeiba,
Mwavutika ja sumaku, mnataka kumbeba,
Kucha hamweshi udaku, hunibidi nende toba,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

Endelea kunicheka, malipo ni duniani,
Ninajua mtachoka, siku moja maishani,
Sitokuwa na wahaka, tanijalia Manani,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

Mwanangu n’tamwelimisha, tulieni mtaona,
Mtapandwa na puresha, mkidhani mie sina,
Nyie zidi kujichosha, natua mie kunena,
Mkata mie mkata, sioni raha mkata.

© Hosea M Namachanja
Milembe, Bungoma, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *