Natamani Utakatifu

Nionyeshe njia yako, njia ile takatifu,
Njia ile ya upako, isokuwa na uchafu,
Huko ndiko nitakako, njia hiyo ya unyofu,
Natamani mimi leo, kuishi kitakatifu.

Leo mimi natamani, kuishi kitakatifu,
Nifanye yake Manani, nami niwe muongofu,
Bwana Yesu awe ndani, nisipate nayo hofu,
Natamani mimi leo, nitende mema mapenzi.

Kama Musa na Haruni, nifanye mambo mazito,
Nitoe maji mwambani, au kwenye kubwa jito,
Niile mana jangwani, n’one chaka lenye moto,
Natamani mimi leo, kuishi kama wa kale.

Niishi kama mitume, niseme neno la Mungu,
Kwa juhudi nijitume, kuokoa walimwengu,
Kweli yote niiseme, hata wanifunge pingu,
Natamani mimi leo, zingerudi zama zile.

Au niwe mchungaji, niongoze waumini,
Niwafanye wakosaji, nao warudi kundini,
Niwabatize kwa maji, wokovu wapate ndani,
Natamani mimi leo, niwe chombo chake Mungu.

Au nipewe karama, ya kutoa unabii,
Ilotoka kwa Karima, niifanye kwa bidii,
Kwa hakika sitagoma, nitafanya kwa utii,
Natamani mimi leo, nikawe kama Eliya.

Au nipewe kipawa, cha kufanya miujiza,
Uponyaji nitagawa, hata kwao maajuza,
Wote sitawapa dawa, hata walio pooza,
Natamani mimi leo, nifanye mambo makubwa.

Au nifanywe mwalimu, niwe mwalimu wa dini,
Nitoe nzuri elimu, hadi wote waamini,
Mola waweze mweshimu, wasibakie dhambini,
Natamani mimi leo, watu waniite Rabi.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *