Haki Zangu Zi Wapi?

Natokeza Wanguwangu, kwa upole utulivu,
Sikiza mswanda wangu, tausema kishupavu,
Zanifinya hizi pingu, ninaishiwa na nguvu,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

Zikisomwa na habari, runingani na redioni,
Waandika wahariri, na habari za huzuni,
Na kisha wanakariri, watu wamekuwa nyani,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

Kweli watu ni wanyama, dhuluma mwanifanyia,
Kuanzia wangu mama, maovu mwanitendea,
Mmenilia na njama, kazi sulubu kufia,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

Ona finyu umbo langu, nazo huruma hamna,
Mwataka kiwili changu, kuharibu ngali mwana,
Mwanishikia na rungu, kubakwa leo na jana,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

Nasikitika ya juzi, kihudhuria mazishi,
Yapata mmoja mwezi, karibu ninakoishi,
Mtoto kavunjwa fizi, na wanyumbani mpishi,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

Vipengele viliundwa, kwa marefu na mapana,
Walakini ni kupondwa, kujiletea laana,
Ninaomba na kulindwa, zangu haki za maana,
Haki zangu ziko wapi, na katiba mliunda.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *