Mke

Mke wa kwanza ni mama, mke ni dada mdogo,
Malizia uhasama, sitake la moyo gogo,
Akitenda ya kuuma, ‘mwondoke’ sizue zogo,
Mke ni kutomchuma, asife ngali pogoo.

Mke mjue mapema, mpe muda usikie,
Limbikiza sifa njema, mpe punje atulie,
Maneno mengi kuzima, na vita uzuilie,
Mke ni kutomchuma, asife ngali pogoo.

Usitilie ya zama,yatanuka kama donda,
Mkeo si wa kukama, wala wa kichapo punda,
Ondoa zote lawama, shika rungu kumlinda,
Mke ni kutomchuma, asife ngali pogoo.

Atendapo yasomema, cheka kisha mwelekeze,
Yatakuwa kama homa, pasi fujo umweleze,
Usitakie kugoma,mahitaji silegeze,
Mke ni kutomchuma, asife ngali pogoo.

Kuwa Mwalimu kusoma, fikira zake kujua,
Tazama wake uzima, kibadilika gundua,
Mpe sifa za uwema,na zeze kumdundia,
Mke ni kutomchuma, asife ngali pogoo.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *