Hadi Lini?

Hadi lini, nitalia, kuchao nikiteseka,
Hadi lini, n’tashangaa, watu wakiimarika,
Hadi lini, tangalia, nikose kusaidika,
Hadi lini, duniani, majuto yataniisha?

Hadi lini, maishani, nitakosa hangaiko,
Hadi lini, masomoni, vitanikwepa vituko,
Hadi lini, safarini, ntaona mteremko,
Hadi lini, duniani, majuto yataniisha?

Hadi lini, tajikuta, nimeipata ajira,
Hadi lini, nitateta, nisipatwe na hasira,
Hadi lini, nitapata, sifanyiwi masihara,
Hadi lini, duniani, majuto yataniisha?

Hadi lini, masahiba, watakuwa wa busara,
Hadi lini, ughuruba, utafikishwa ahera,
Hadi lini, nitabeba, mavazi yangu chakara,
Hadi lini, duniani, majuto yataniisha?

Hadi lini, njia zangu, zitaweza kufunguka,
Hadi lini, sala zangu, zitaweza kujibika,
Hadi lini, hali yangu, itaja kubadilika,
Hadi lini, duniani, majuto yataniisha?

© Hosea M Namachanja

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *