Duniani Hakuna Mkweli

Dunia kweli dunia, waja wamebadilika,
Macho wameyavumbia, maovu yanotendeka,
Wongo wamepalilia, na utu umetoweka,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

Makasisi kanisani, nao hawaaminiki,
Wamehini waumini, kuwafanya mashabiki,
Ushuhuda kanisani, hata hausadikiki,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

Mahakama yahukumu, wasiotenda maovu,
Kadhongo kwake hakimu, hubadili mtenda ovu,
Uhalalisha haramu, kuendekeza maovu,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

Madaktari na manesi, hawaaminiki pia,
Wamekuwa ibilisi, magonjwa kudanganyia,
Hekima wameiasi, pesa wanaparamia,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

Wanabiashara pia, wamepunja wanunuzi,
Wengi wanawahadaa, waja wasio ujuzi,
Huuza ghushi bidhaa, kwa bei iliyo ngazi,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

Wanahabari wauni, wanatunga uongo pia,
Propaganda redioni, hamaki kupalilia,
Porojo magazetini, na wongo kuenezea,
Kweli hakuna mkweli, binadamu ni waongo.

© Justine Bin Orenge

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *