Njiwa Peleka Salamu

Jamali yalimfika, ikambidi aseme,
Alala aweweseka, japo akaza kiume,
Ujumbe kauandika, salamu zake atume,
Njiwa salamu peleka, kampe wake Mwasiti.

Yalimjaa madhila, machozi tele usoni,
Aligoma hata kula, huzuni ipo moyoni,
Yeye kwake ndo chakula, kwa hilo wala haguni,
Njiwa katumwa salamu, aseme amhitaji.

Kasema ameshatekwa, na kweli alitekeka,
Alipotaka kuwekwa, hakika aliwekeka,
Kama ni moyo kushikwa, sibishi alishikika,
Njiwa katumwa haraka, fikishe ujumbe wake

Aliachwa peke yake, kwani alikosa nini?
Akabakia mpweke, na mwanga tena haoni,
Kweli lile sekeseke, lilimu’ma kama nini,
Njiwa katumwa salamu,zimfikie Mwasiti.

Bora angepigwa rungu, likatua utosini,
Au angetiwa pingu, akafungwe gerezani,
Anye anye kwa mafungu, kwa choo cha pembezoni,
Njiwa kweli katumika , ‘peleke kilio chake.

Kapewa zake salamu, kasema amhitaji,
Asije jinywea sumu, akamkosa mwu’mbaji,
Akaendea jahimu, ambapo apahitaji,
Njiwa katumwa salamu, aseme amhitaji.

Hapa sasa nahitimu, wino umeshatindika,
Hizi ndo zake salamu, nami mwisho nimefika,
Jamali kajawa hamu, penzi bado alitaka,
kampe zake salamu, njiwa haraka peleka.

© Kinyafu Marcos, 2018.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *