Gwiji Limetutoka

Afrika ni kilio, twende wapi kujipoza,
Hatunalo kimbilio, nani aje tuliwaza,
Ndio imekuwa sio, tunabaki tunawaza,
Koffi gwiji amekwenda, hazina imeondoka.

Tanzania hadi Ghana, ni majonzi si utani,
Wapi tena tutakwona, umetwacha na huzuni,
Sura zetu zasonona, twaumia mitimani,
Koffi gwiji amekwenda, nyoyo zimetupondeka

Kenya Rwanda na Burundi, nao sasa wanalia,
Wampate wapi fundi, aletumwa na Jalia,
Sasa mbele hawaendi,amani waililia,
Koffi gwiji amekwenda, bado sisi twakutaka.

Tuliona nguvu zako, pande zote duniani,
Hukupenda chokochoko, ulidumisha amani,
Njema ile kazi yako, ukalipwe na Manani,
Koffi gwiji amekwenda, nenda baba pumzika.

Afrika bara letu, limejawa na simanzi,
Umetwacha peke yetu, tumejawa majonzi,
Tuliona wako utu, na lako zuri lako penzi,
Koffi gwiji amekwenda, shujaa wa Afrika.

Hatunalo la kusema, nenda baba kwa heshima,
Japo nyoyo zazizima, mshumaa umezima,
Nenda lala pale pema, kwa mapenzi ya Karima,
Koffi gwiji umekwenda, furaha imetoweka.

© Kinyafu Marcos

Maoni 1

 1. Abed

  guso la moyo yakini,
  guso lachoma moyoni,
  ni mshale wenye sumu,
  mrefu vujo la damu,
  kumbuko lililo kuntu,
  Gwiji wetu wa kibantu,
  Pahala pema ulale,
  Nasi twaja polepole.

  Jibu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *