Ushairi

Shairi hung’aa, kwa ustadi utungapo,
Jema kuandaa, ushairi mwema upo,
Watu huduwaa, jema uliandikapo.

Haki itetee, usalama uwe kwako,
Tamu liwekee, japo vina vema viko,
Sifa zingojee, kwa umaarufu wako.

Waja elimisha, kupitia kwa shairi,
Bila kuwatisha, waelimishe ni heri,
Koja kukuvisha, halitakuwa la siri.

Mabaya waonye, bongo zao zionyeke,
Waja uwakanye, mema peke yatendeke,
Beti zikusanye, za maonyo uandike,

Watu waarifu, kupitia kwa ubeti,
Wa kusifu sifu, uandikapo kwa hati,
Watoe upofu, itakuwa ni bahati.

Watu changamsha, wadhiha waweze cheka,
Mema ukipasha, lazima kuchangamka,
Ubeti watosha, wacheke wakianguka.

Tunga kwa heshima, pasi matusi kufoka,
Taadhima sema, usemi mwema andika,
Usiseme lawama, mwanadamu kuteseka.

Oneka liweze, dhahiri lidhihirishe,
Lako litangaze, waziwazi lionyeshe,
Usilipoteze, hadharani ulipashe.

© Kimani wa Mbogo

 

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *