Utokako Ukuole

Yawaze yalokingama, uyasanifishe tele,
Usikose fanya wema, hisani uwafanyile,
Ijapofika kiyama, usiwe na la matule,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Likopanda vingulima, kosa usilirudile,
Chiniyo ukatazama. wendapo fika kilele,
Ulikopita dhalama, ola usiwe mtule,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Yarekebishe ya zama, usirudie yajile,
Usiyatende mafama, maovu kuliko mbele,
Baraka hukuandama, uwapo mwema mpole,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Ikufatapo neema, ukaukosa uwele,
Usikose kuinama, magoti umpigile,
Umshukuru Karima, umhishimu vivile,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

Awapo nayo hikima, hakosi jema nenole,
Ajapofika kukwama, huyatizama ya kale,
Paovu atalalama, akaandama miale,
Ufikapo kaditama, utokako ukuole.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *