Ninalo Jambo Muhimu

Ujualo ni msimu, ukidhani linafana,
Mwamuzi una jukumu, kutatua yako dhana,
Hadi siku za kuzimu, tatizo mtapambana,
Ninalo jambo muhimu, kuliko unaloona.

Lolote walifahamu, hisia kuziumbuwa,
Tambua ni yako zamu, kunga zote kuzijuwa,
Una shida kujikimu, za wengine watambuwa,
Ninalo jambo muhimu, kuliko unalojuwa.

Lijue lako jukumu, ulienzi kwa makini,
Liwate lenye hukumu, kwao usiothamini,
Watu wasikulaumu, ya kwao ukitamani,
Ninalo jambo muhimu, kuliko unalodhani.

Umeshashika hatamu, kuchunguza ya kuvuma,
Kumbe ndiyo yako zamu, kutwa moja utakwama,
Wengine kuwatuhumu, huenda huna rehema,
Ninalo jambo muhimu, kuliko unalosema.

Imekuingia hamu, lengo lako kuwapiku,
Hujui hujahitimu, kwa huo wako udaku,
Heshima ni la kudumu, mchana ama usiku,
Ninalo jambo muhimu, kuliko unaloshuku.

© Kĩmani wa Mbogo
(Mwanagenzi Mtafiti)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *