Ninaomba Mnijuze

Zipo wapi zama zile, zama zile za zamani,
Zamani zile za kale, mbona sasa sizioni,
Sizioni hata kule, siulizi kwa utani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Tulipewa visa kale, na hadithi za kubuni,
Walobuni visa vile, wapo wapi nambieni,
Walitoa visa tele, tele iso na kifani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Walokuwa nazo ndwele, walienda vilingeni,
Walichanjwa nyingi chale, chale hadi ulimini,
Yakawaisha mapele, yalokuwa miilini,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Ugali kwalo tembele, tulitenga mkekani,
Na samaki wa kambale, tuliwavua mitoni,
Natamani mambo yale, yangerudi majumbani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Uji ule wa mchele, ulouzwa mashuleni,
Nao mkate wa gole, mbona hauonekani?,
Kababu zenye uzile, ziwapi nazitamani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Nauliza kwa upole, jibuni nyie waneni,
Siulizi kwa kelele, nitoe zenu imani,
Yanichezile machale, nawaza miye jamani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

Yangu yote nisemile, yalokuwa mtimani,
Nijuzeni polepole, nielewe kwa undani
Sitishiki na mishale, miye kubwa la manyani,
Zipo wapi zama zile, ninaomba nijuzeni.

© Kinyafu Marcos, 2018.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *