Mwana Kilimilimi

Hivi nini unapata, mdaku nakuuliza,
Mambo yakukereketa, hukomi kuyaeleza,
Kila unalolipata, mapema walisambaza,
Udaku sio ujuzi, ebu acha hiyo kazi.

Upo kama tarumbeta, kelele unaeneza,
Pande zote unapita, umbeya kuutangaza,
Mambo unayoyaleta, mwenziyo wanichukiza,
Udaku sio ujuzi, ebu acha hiyo kazi.

Unapenda usalata, umbeya kuufanyiza,
Nyatunyatu kama bata, madogo unayakuza,
Sikupendi katakata, mdaku wanichefuza,
Udaku sio ujuzi , ebu acha hiyo kazi.

Bora ukauze mbata, ama ukauze pweza,
Ama viazi mbatata, pato uweze ongeza,
Ila si kubwata bwata, mwenziyo unanikwaza,
Udaku sio ujuzi, ebu acha hiyo kazi.

Maana kinachofwata, sasa nitakubamiza,
Siku nikikukamata, kweli nitakuchaza,
Wewe leta za kuleta, kama sijakuumiza,
Udaku sio ujuzi, ebu acha hiyo kazi.

© Kinyafu Marcos.
(MUUMINI WA KWELI)

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *