Mji wa Ajabu

Nilitoka mashambani, kujiendea mjini,
Na mfuko mabegani, na tunguri mkononi,
Kwa tabasamu kinywani, kwa maisha ya mjini,
Jamani singeambika, Lo! Mji una wenyewe.

Nikatua kituoni, kwa kishindo cha mwilini,
Nikaabiri basini, kujiketia kitini,
Na karibu dirishani, kasonga pale pembeni,
Kicheko kilijazika, kuwaaga wa shambani.

Matwana hiyo mbioni, kutifua mavumbini,
Dereva ‘ hadaratini, nayo mirungi kinywani,
Kijipombe kichupani, mziki wa ujanani,
Hili basi la mjini, tofauti la shambani.

Nikafikia jijini, mji niliotamani,
Nikaenda msalani, nikasimame pembeni,
Ala! Pesa mkononi, ikabidi nilipeni,
Ni maajabu ya jiji, waja kuzipenda hela.

Mngurumo wa tumboni, ishara kuwa njaani,
Miayo mingi kinywani, na hamu kubwa mateni,
Kufikiria fikirani, nunue maji dukani,
Jamani bidhaa mji, maradufu bei rafu.

Na kelele umatini, huyo mwizi mshikeni,
Kijana wa hirimuni, kakimbizwa chochoroni,
Akachapwa mgongoni, kichwani na tumboni,
Kumbe waja wa mjini, sheria i mikononi!

Kashitushwa na mjini, raha nisiwe moyoni,
Hapa ndo nikaamini, kumbe mji ni shuleni,
Maisha ni kwa mapeni, kando sana na shambani,
Kajitoma tena ndani, nirudi kwetu nyumbani.

Sirudi tena jamani, nyumbani ndiko nyumbani,
Hata kama si pangoni, nitaishi kutamani,
Ugali wa mawimbini, ninywe uji mihogoni,
Do! Nyumbani ni nyumbani, hata kama ni pangoni.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *