Taiti Tatizi

Ijapo si mtambaji, nitakuli kwa katiti,
Wala sitafuti taji, musinipige vijiti,
Ningependa kuwahoji, hawa wavaa taiti,
Zingwizingwi lipe nguo, uyaone mashauo.

Imekubali jasadi, kila kona umejaza,
Kula umejitahidi, chochote hukukisaza,
Sijui lako kusudi, taiti kujiingiza,
Zingwizingwi lipe nguo, uyaone mashauo.

Wengine na njorinjori, miguu falau twiga,
Taiti hutia shari, daliji wanapoiga,
Utadhani watiriri, wenyewe wamejiroga,
Zingwizingwi lipe nguo, uyaone mashauo.

Mavazi mnayovaa, yadhihirishe heshima,
Hivyo yawe yakufaa, muziepuke tuhuma,
Mutakuja zua baa, na kuzikosa rehema,
Zingwizingwi lipe nguo, uyaone mashauo.

© Moses Chesire
(Sumu ya waridi) Kitale, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *