Nyoka wa Ndumakuwili

Mahuluku vimelea, watu hawatabiriki,
Leo akuchekelea, mkate mkishiriki,
Kesho akakukemea, urafiki kutaliki,
Nyoka wa ndumakuwili.

Huuma akivuvia, nyoka wa ndumakuwili,
Huku anakusifia, chuo ulivyohafili,
Sifa anazomwagia, nyingi isiyo kalili,
Nyoka wa ndumakuwili.

Ina mema na maovu, huu ndio ulimwengu,
Ina maji na pakavu, penye amani na bangu,
Wapo walio chakavu, gambani miba za ningu,
Nyoka wa ndumakuwili.

Tahadhari mahuluku, kaa nao kimtindo,
Husiana kisukuku, mtu pweke ni uvundo,
Hawapendi uwapiku, cheo ukiweke kando,
Nyoka wa ndumakuwili.

Fundabeka langu paja, tunzie lisivunjike,
Sihofu mambo kangaja, na mimi nitajirike,
Mungu fanya tafirija, adui wasilimike,
Nyoka wa ndumakuwili.

© Uledi Bryan
(Kinda Mtunga Nudhumu)Nakuru, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *