Elimu Bora

Naingia ukumbini, niyaseme ya elimu,
Elimu yenye dhamani, kwa waja wote muhimu,
Kwa maisha ya usoni, kurahisisha magumu,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Mawasiliano bora, elimu huangazia,
Utangamano imara, nyumbani na shule pia,
Elimu yenye ubora, jamii huizindua,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Elimu ya kukariri, hoja kweli haifai,
Hutoa madaktari, walo viza ja mayai,
Wakakosa umahiri, tiba bora hawatoi,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Elimu ya kimaisha, ndio elimu faafu,
Heshima huifundisha, pamoja na utiifu,
Mja kumkamilisha, akawa mkamilifu,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Ni vyema kujitambua, na tena kujiamini,
Vipaji kuvitumia,alotupea manani,
Ajira kutupatia, na nafasi maishani,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Nidhamu ni ya maana, wasomi kuzingatia,
Ndipo mpate kufana, na kuipiga hatua,
Changamoto kikutana, lazima kuvumilia,
Elimu bora ni ile, elimu ya kimaisha.

Bonface Wafula
(Mwana wa Tina) Nakuru, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *