Lugha Chafu Lugha Gani?

Ninaomba usikie, hizi lugha niambie,
Maswali niulizie, na kisha unijibie,
Pia nifafanulie, na nyuma nisisalie,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Mama kuitwa Mathee, baba kuitwa fathee,
Mji kuitwa kambee, mwanamme mzaee,
Kalenjini mkalee, Kikuyu msaperee,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Ugua ni kugonjeka, hiki kweli Kiswahili?
Hili neno kusondeka, jamani litupe mbali,
Yasome maneno fika, tupa maneno makali,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Nini maana lisaa, na wengine ni masaa,
Ni vyema kusema saa, ili kutupa balaa,
Jimulike kama taa, lugha ibaki kung’aa,
Lugha hizi lugha gani,vijana mwatusemea?

Mbwa kuitwa umbwa, ni neno bila mpango,
Ni kiumbe aliumbwa, pasi wako mchango,
Heri neno kuambwa, vyema bila ya uongo,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Aisee naulizeni, nani kweka stempu?
Ati kwenda msalani, kuwa ni kwenda kupupu,
Ninatiwa hasirani, naumwa kama majipu,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Na pesa kuitwa doo, mkidai ni usasa,
Mia Moja nayo soo, roho yangu wakukusa,
Kusinywa ni kuboo, havikomi vyenu visa,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Naomba kujizatiti, vijana pate hekima,
Kuiunda mikakati, kujua maneno wima,
Nakomeza zangu beti, na kwa lugha ya heshima,
Lugha hizi lugha gani, vijana mwatusemea?

Mwangi wa Gĩthĩnji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *