Tajiri wa Huzuni

Mola wangu ewe Mola, sikia changu kilio,
Mehangaikia dola,sijapata wangu mlo,
Mepoteza motorola, siwezi kusema halo,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Niliyemwita kipenzi, hivi sasa ni shubiri,
Ameenda kwenye enzi, ya wampao sukari,
Kisa hatuli viazi, kaenda bila habari,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Mimi changu kibarua, kuokota takataka,
Nayajaza magunia, pomoni bila mipaka,
Ndipo nitapata mia, ama nipewe nafaka,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Ndugu zangu majirani, wanitenga ka ukoma,
Wa bara hadi pwani, wanisema kwenye ngoma,
Mimi niko taabani, angalau ningesoma,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Wanibeza watoto, kwa kuniita tahira,
Wamekuwa kama moto, lini tapata ajira,
Maisha kama kokoto, ndio wangu ujira,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Narudi kwako Rabana, wewe mtoa riziki,
Sitaki mi kujifanya, kama wenye pikipiki,
Nisamehe ewe Bwana, niepushe na mikiki,
Mi maskini wa mali, ni tajiri wa huzuni.

Emmanuel Charo ( Malenga Daktari)
Chuo Kikuu cha Meru, Kenya

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *