Mla Nawe Hafi Nawe

Ndugu vyema ni kutii, haswa ukitii ndugu,
Dada yako kumtii, sifanye tabia sugu,
Mpe heshima sahii, simfyeke kama gugu,
Mla nawe hafi nawe, ila mzaliwa nawe.

Ndugu wako wa kiume, ndugu yule ndugu kaka,
Usimchome kwa sime, wala kukatia shoka,
Mpe ari pate shime, mali mengi mkisaka,
Mla nawe hafi nawe, Ila mzaliwa nawe.

Ukitaka msaada, omba kwanza ndugu yako,
Umlipe hiyo ada, bila kuleta vituko,
Zaidi akiwa dada, mpe hadi ongezeko,
Mla nawe hafi nawe, ila mzaliwa nawe.

Undugu ni kufaana, Wala sio kufanana,
Aibu ni kufichana, mambo yalo ya maana,
Kisasi kulipizana, jambo lisilo thamana,
Mla nawe hafi nawe, ila mzaliwa nawe.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *