Uswahilini Kwetu

Tuli natulia chini, nudhumu kuiandika,
Niseme ya mtaani, jinsi yanavyo fanyika,
Mambo ya uswahilini, matendo yan’otendeka,
Waswahili wana nini, mwezenu jibu nataka.

Uwakute mkekani, wakaa pakakalika,
‘Tasema wafanya nini, jinsi walivyo zunguka,
Kumbe wapo umbeani, mmoja anasemeka,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu nataka.

Nguo juu magotini, ndo mitoko wanatoka,
Vipima joto kwapani, vipodozi wameweka,
Wanja poda na hereni, na vingine kadhalika,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu nataka.

Wanashinda ulabuni, vileo wanaleweka,
Haya wala hawaoni, chupa zao wakishika,
Si mchana si jioni, mtaani hekaheka,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu nataka.

Kutwa nzima kijiweni, humo kambi wanaweka,
Bangi zipo vidoleni, moshi nao unafuka,
Madhara hawayaoni, uhuni umewateka,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu nataka.

Juzi kwa Ngengemkeni, kama waenda kwa Beka,
Pale kwao chochoroni, niliwakuta vibaka,
Wakanipiga kichwani, na ngeu wakaniweka,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu mataka.

Haya nawaambieni, siyo ya kufikirika,
Waja kweli aminini, mtaa nimeuchoka,
Naomba nishaurini, tiba inahitajika,
Waswahili wana nini, mwenzenu jibu nataka.

© Kinyafu Marcos,2018.
(Muumini wa kweli)
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *