Riziki Haina Kwao

Riziki haina kwao, mwenzenu nimeamini,
Hupata wajaliwao, kutoka kwa Mkawini,
Pasina upendeleo, waja embu eleweni,
Walo wakinuka vumba, sasa wapo ambarini.

Hugawa anapotaka, kwa yeyote duniani,
Siku yako ikifika, bahati itaja ndani,
Haiwezi zuilika, hata angesema nani,
Walo wakinuka vumba, sasa wapo ambarini.

Usije kukurupuka, kutamani vya jirani,
Tamaa ikakuteka, ukatia mfukoni,
Utaja kuaibika, uchekwe pasi kifani,
Usiiogope vumba, utaenda ambarini.

Wala ‘siwe na haraka, mwamini yeye Dayani,
Haraka h’ina baraka, liweke hili kichwani,
‘Tapata unachotaka, utafurahi moyoni,
Hutanuka tena vumba, utaenda ambarini.

Mja usije kuchoka, kutafuta asilani,
Usijali wan’ocheka, na kejeli mitaani,
Waache wakiboboka, wewe mwamini Manani,
Walo wakinuka vumba, watakuwa ambarini.

© Kinyafu Marcos,2018
Dar es salaam,Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *