Mtenda Anapotendwa

Uliyaanza mwenyewe, na tena huku wacheka,
Ukarusha sana mawe, bila ya kuwa na shaka,
Vipi yakufike wewe, uanze kukasirika?
Mtenda anapotendwa, huona katendwa sana.

Uliona ni furaha, kufanya yakafanyika,
Moyo ulijawa raha, isiyo ya kupimika,
Leo waona karaha, kwako yalipokufika,
Mtenda anapotendwa, huona katendwa sana.

Kwa nuio ulitenda, sio kwa kughafilika,
Ulitenda kwa kupenda, kwa watu wakila rika,
Iweje yamekushinda, waanza kukabaika?
Mtenda anapotendwa, huona katendwa sana.

Umejawa uhasidi, usoweza elezeka,
Mawi yaso na idadi, kwa wengi yametendeka,
Sasa leo huna budi, na wewe kufedheheka,
Mtenda anapotendwa huona katendwa sana.

Nakuhasa mkaidi, ni heri kubadilika,
Mwenyewe wewe shahidi, jinsi unavyoteseka,
Safisha wako fuadi, leo utatakasika,
Mtenda anapotendwa, huona katendwa sana.

© Kinyafu Marcos, 2018
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *