Heri Dooteni

Siwezi kuuma chanda, miye niwe na sononi,
Kisa ubavu kupinda, ni kufuru kwa Manani,
Humpa anayependa, kwa urefu na uzani,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Haya nilopata shinda, nayaona ya thamani,
Wala sitamani kenda, moja yangu naamini,
Sitaki twishwa ja punda, mwili uwe taabani,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Kwa nongo anonikanda, si nyongeki asilani,
Eti nimepewa nganda,si mtaji mchezoni,
Wala siwezi kukonda,ni jaza yake Rabani,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Hata nikipewa donda, tawinga inzi pembeni,
Kwa majimoto takanda, niipate ahueni,
Vya watu sito vipenda, changu nikifanye duni,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Juu siwezi kupanda, nilipo niafueni,
Hata ipulizwe panda, mnaopanda pandeni,
Kwa haya niliyo funda, naitoa shukurani,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Jua linazidi kwenda, inayofwata jioni,
Dhima ya yangu agenda, vya wengine sitamani,
Bura yangu naipenda, si badili kwa rehani,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

Kaditamati na kwenda, neno liko ukingoni,
Mlo wagonjwa wa inda, hino tiba nakupeni,
Mimi cha kamba kitanda, thamani yangu mwishoni,
Afadhali dooteni, kama ambari kutanda.

© Hamisi A. S. Kissamvu
Baitu shi’ri, Mabibo, Dar es Salaam

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *