Aambuaye Unyayo

Kwa kuinuwa unyayo, kwa heri au kwa shari,
Ukaupiga na moyo, kuitimiza dhamiri,
Umeianza niayo, waonaji wa subiri,
Aambuaye unyayo, ameianza safari.

Umeisema haliyo, ya mbele ukadabiri,
Ukakiweka kingayo, kufanya sana dhikiri
Wasojua ulonayo, hawafanyi tafakari
Aambuaye unyayo, ameianza safari.

Aloinua unyayo, ana alo tanadhari,
Hawezi piga miayo, kama aliye jibari,
Hakosi mazingatiyo, katika yake safari,
Aambuaye unyayo, ameianza safari.

Alonajicho la choyo, hamuombeyi mazuri,
Huzifuta zake nyayo, na kuzitia dosari,
Haimdhuru filayo, kwa nguvu zake Ghafari,
Aambuaye unyayo, ameianza safari.

Kuyacheka yaendayo, uvivu wa kufikiri,
Mazuri tuyaonayo, yalishatiwa makiri,
Nikusubiri yajayo, siyo tuanze bashiri,
Aambuye unyayo ameianza safari.

© Hamisi A. S. Kissamvu
Baitu shi’ri, Mabibo, Dar es Salaam

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *