Una Howe Gani?

Kwa jinalo Rahamani, niponye wangu mtima,
Niikwepe mitihani, leo na kesho kiama,
Howe ilo na thamani, kwaye alofanya, vyema
Howe ya mwenye kufuma, wewe una howe gani?

Maneno tele kinywani, hatuoni ulofuma,
Unataka usukani, na siye tukae nyuma,
Hebu sema hadharani, ulounda yakakwima,
Howe ya mwenye kufuma, wewe una howe gani?

Tuonayo ya zamani, wapi yako muadhama,
Tukasema marijani, tukipambe kwa heshima,
Hilati zimesheheni, kama mtego wa nyama
Howe ya mwenye kufuma, wewe una howe gani?

Tadabiri hatuoni, walau iwe alama,
Tukafurahi waoni, kama kiigizo chema,
Hovyo haipatikani, bila jambo la heshima,
Howe ya mwenye kufuma wewe una howe gani?

Gozi lipo uwanjani, uyafanyayo mafama,
Weka kitu kimiani, wasemaji watasema,
Hausifiki fanani, kama huna jambo jema,
Howe ya mwenye kufuma wewe una howe gani?

Haya ni ya hadharani, hayafichiki daima,
Ja pembe za hayawani, vile zinavyo simama,
Twambie umefanyani, howe tusije kunyima,
Howe ya mwenye kufuma wewe una howe gani?

Beti ziko ukingoni,tungo yaenda kukoma,
Mtu havishwi nishani, pasi kuacha alama,
Anowahi kisimani, hunywa yalio tuwama,
Howe ya mwenye kufuma wewe una howe gani?

© Hamisi A. S. Kissamvu
Baitu shi’ri, Mabibo, Dar es Salaam

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *