Koti la Babu

Koti la babu l’na chawa, ingawa sina uchafu,
Ni mengi ninayajuwa, mema na yenye udufu,
Mengine huyatumbuwa, k’ma utamu wa dafu,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Kila n’kiwa safari, n’kiwa mgaagaa,
Duniani k’safiri, ulimwengu kutambaa,
Sharti kutahadhari, iniishie tamaa,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Ukiwa na walimwengu, tahadhari ulimiyo,
Mafunzo yote ya tangu, ni heri kutambuliyo,
Usiyazue machungu, matamshi machafuyo,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Ni busara kunenewa, kushinda kuneneana,
Usipende kusikiwa, pendea kusikizana,
Heshima h’taishiwa, wala hamtakosana,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Kuyaona ya kuona, uyaone yale mema,
Yale mawi kuyakana, uyatupe kuyatema,
Uyatake yak’fana, mithili babu wa zama,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Mlimwengu mwenye macho, haarifiwi ‘tazame,
Hekima kupata kocho, na dhana kama umeme,
Chochote ukipatacho, ni busara uk’pime,
Koti hili ni la babu, koti halikosi chawa.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *