Methali Zasifu na Kukashifu

Kurudi narudi hima, kwenu kumwaga busara,
Nimwage yangu hekima, hata yakiwa yakera,
Shika n’takayosema, kichwa ni ya mja dira,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

Polepole ndio mwendo, kwa yote ukiyatenda,
Ikiwa hata upendo, kwa lile usolipenda,
Luchunguze hilo tendo, hasara ‘sije kutanda,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

Ada ya mja kunena, kwa mwungwana ni vitendo,
Sema yalo ya maana, yaso ma’na weka kando,
Ni muhimu kukazana, usinaswe kiutando,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

Mpiga ngumi ukuta, huumiza mkonowe,
Mja kujipa matata, kujiumiza mwishowe,
Anabaki ni kuteta, lugha gani asemewe,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

Mwenye macho haambiwi, haambiliwi tazama,
Hata akawa kiziwi, huyaona ninasema,
Kwa maovu hutakiwi, kukataliwa ni vyema,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

Mcheza kwao hutuzwa, akituzwa hutuzika,
Ususie kupumbazwa, usije kutatizika,
Pendelea kufunizwa, methali kumithilika,
‘Kwishi si Moja methali, za sifu na kukashifu.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Maoni 4

 1. Alvin Aron

  Asotaka la mkuu, guu lake alivunja,
  ‘sijione uko juu, kwazo fegi nazo ganja,
  Au kutaka makuu, kuruka vyote viwanja,
  Kumbuka u kuukuu, ipo siku utadanja.

  Safi sana, shairi tamu ndugu

  Jibu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *