Msela Asokwepeka

Lazima a’che vilio, michozi kutiririka,
Bongo zipate tindio, yani akili kuruka,
Butwaa na mishangao, isoweza elezeka,
Msela asokwepeka, msela hana mafao.

Atayajia makao, siku yake ikifika,
Kwenye wengi wakaao, kipenzi kitatoweka,
Kwa haraka mbiombio, furaha itaondoka,
Msela asokwepeka, msela hana mafao.

Pasipo matarajio, sherehe itafanyika,
Na nyimbo za mapambio, kumsihi Marabuka,
Liwe lake azimio, hali pema kumuweka,
Msela asokwepeka, msela hana mafao.

Mwisho huwa ni tukio, la kipenzi kumzika,
Kama jua ni machweo, ama moto kuzimika,
Kumbuka ni tangulio, msela hajatosheka,
Msela asokwepeka, msela hana mafao.

Kama unalo sikio, sikia na elimika,
Kwa wale waabudio, abudu na salimika,
Jua huna kimbilio, msela kumuepuka,
Msela asokwepeka, msela hana mafao.

© Alvin Aron
Tunevin, Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *