Urembo Wako si Chochote

Kipusa una vituko, twaviola hadharani,
Vyanambukiza udhiko, nikaliweka tungoni,
Vimekupumbaza vyako, wakuu wakulaani,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

Kitwani zavurungana, si zetu si za kigeni,
Nywele zaangukiana, kisogo na utosini,
Ukadhani unafana, wende zako kinarani,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

Wajihi wajipodowa, podari imo usoni,
Sana umejikwatuwa, ukijeleza rohoni,
Dhahiri hujang’amuwa, umaridadi hunani,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

Maziwa yalaliana, huna umbo kifuani,
Miguu wima haina, walakini kiunoni,
Urembo huna maana, kipusa-mtu hufani,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

Kuchani unayo hina, vipuli masikioni,
Kipini chaonekana, wekundu umo domoni,
La urembo ndilo huna, kawoneshe kinarani,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

Wadhani umerembeka, uwaoneshe halani,
Miye nishaghadhabika, nikikuona matoni,
Kumbe hujabusurika, welevuke ubongoni,
Urembo wako siwoni, si chochote si lolote.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *