Jembe Jipya

Unashiriki maombi, na ibada takatifu,
Wachota nyayo za vumbi, sangoma ‘kikutarifu,
Tena ujawa vitimbi, kwa matusi lugha chafu,
Jembe jipya sikuwezi.

Watubisha watu dhambi, tena huwapa wakfu,
Lakini wachinja jimbi, zindiko kwa walo wafu,
Imara yako filimbi, kuzini muadilifu,
Jembe jipya sikuwezi.

Nyingine wala huimbi, ila Mola kumsifu,
Jioni kwa mkunumbi, wayapeleka madafu,
Usiku zako ni kumbi, za Mungu kumkashifu,
Jembe jipya sikuwezi.

Kwa biblia sio pimbi, wajua na msahafu,
Waganga ka’ kumbikumbi, wawajua kisanifu,
Unatoka na kitambi, vilevi vi kwa jokofu,
Jembe jipya sikuwezi.

© Alvin Aron
Tunevin, Dar es Salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *