Za Kale Dhahabu

Walikuwa kama sisi, duniani humuhumu,
Hawakupenda maasi, waliishi kwa nidhamu,
Matendo yote meusi, hawakuyapa sehemu,
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

Waliishi kwa upole, tena kwazo sifa njema,
Vijana wa enzi zile, walisifika kwa wema,
Hakuwependa kelele, walinena kwa hekima
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

Ni kweli walisifika, jamii iliwapenda,
Kwa wote walipendeka, hakuna aliyeponda,
Walipambana hakika, mabaya wakayashinda,
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

Zilidumu ndoa zao, sote tunashuhudia,
Zipo hai hata leo, waama twajionea,
Twende tujifunze kwao, hazina kujipatia,
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

Wazee tuwaheshimu, ili tupate baraka,
Wala tusiwashutumu, hata wakighafilika,
Mema tusijidhulumu, mabaya yakatufika,
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

Hapa sasa nakomea, tamati nimeshafika,
Haya ni’lowaambia, tusiache kuyashika,
Tuzidi kuwaombea, wazee bila kuchoka,
Wazee wana hazina, twende tujifunze kwao.

© Kinyafu Marcos,2018.
Dar es salaam,Tanzania.

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Your email address will not be published. Required fields are marked *